
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wanawake waliobahatika kupata fursa ya elimu na kuwa viongozi kwenye maeneo mbalimbali, wasisahau wajibu wao wa malezi kwa watoto watoto ili kuwaepusha kujiingiza kwenye mienendo isiyofaa.
Ameyasema hayo leo kwenye maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanza kwa Mafunzo ya Uongozi kwa Wanawake Tanzania (Female Future Program) sambamba na Mahafali ya Wahitimu wa Awamu ya 10 ya Mafunzo hayo na Mkutano wa 7 wa Uongozi, yaliyofanyika katika ukumbi wa The Super Dome.
“Haitegemewi kuwa msomi au nafasi ya kiuongozi unayoipata mwanamke iwe sababu ya kuvuruga familia au kuharibu watoto wake,” amesema.
Aidha, Rais Samia ametoa wito kwa wanawake kudhihirisha ushupavu wa uongozi kwenye Mashirika na Taasisi mbalimbali na kuwataka kuwa wabunifu kwenye kazi zao na kuwa waaminifu katika kulipa kodi ili kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali inayogusa maisha ya mwananchi.
Sambamba na hilo, amewataka wanawake kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu ili kuongeza imani na amani kwa jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.