Rais Dk Magufuli atoa elimu ya viwanda kwa maafisa wa SADC

0
41

Rais Dk Magufuli amebainisha kuwa nchi za SADC zimeendelea kuwa wazalishaji wa malighafi na nguvu kazi kwa ajili ya mataifa mengine huku zenyewe zikiwa waagizaji wa bidhaa za viwandani kutoka nje ilihali zikipangiwa bei ya kuuza na kununua bidhaa hizo, hali inayodidimiza wakulima na kurudisha nyuma juhudi za kupata maendeleo ya kiuchumi.

Ameyasema hayo leo wakati akifungua maonesho ya 4 ya wiki ya viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na kuhimiza nchi wanachama kutilia mkazo utekelezaji wa Mkakati wa SADC wa Maendeleo ya Viwanda wa kuanzia mwaka 2015 – 2063.

Ameongeza kuwa kutokana na kutokuwa na viwanda urari wa biashara kati ya Afrika na mabara mengine umekuwa sio mzuri na ametolea mfano wa mwaka 2017 ambapo thamani ya biashara kati ya Afrika na Umoja wa Ulaya ilikuwa ni shilingi Trilioni 708 (Euro Bilioni 280) ambapo Afrika ilinunua bidhaa za shilingi Trilioni 376.7 (Euro Bilioni 149) na ikauza bidhaa za shilingi Trilioni 331 (Euro Bilioni 131), lakini asilimia 60 ya bidhaa ilizouza zilikuwa ghafi na hivyo kuwa na thamani ndogo.

Hii inathibitisha kwamba sisi Afrika tunazalisha bidhaa ambazo hatuzitumii na tunatumia bidhaa ambazo hatuzizalishi, ni lazima tubadilishe mwelekeo huu ili tuzalishe bidhaa ghafi, tuzisindike au kutengeneza viwandani na tuzitumie

Ili kuepukana na changamoto hii inayosababisha upotevu wa fedha za kigeni, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa nchi za SADC kutekeleza kwa vitendo nguzo 3 za Mkakati wa SADC wa Maendeleo ya Viwanda ambazo ni kuhimiza maendeleo ya viwanda kama kichocheo cha mageuzi ya kiuchumi na kiteknolojia, kuongeza ushindani wa bidhaa za viwandani na kutumia mtangamano wa kikanda na jiografia yetu (yenye watu takribani Milioni 350) kwa maendeleo ya viwanda na uchumi.

Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa nchi za SADC kuweka kipaumbele katika uhawilishaji wa teknolojia ya viwanda vya ndani ya Jumuiya na ndani ya Afrika pamoja na kuuziana malighafi na bidhaa zingine miongoni mwa nchi wanachama ili kukuza mitaji na kuendeleza viwanda vya ndani ya SADC na Afrika nzima, kukuza na kuendeleza ubunifu wa watu wa Afrika pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia rahisi na kujenga mazingira wezeshi kwa ajili ya kukuza sekta ya viwanda.

Maeneo mengine ni kuondoa vikwazo vyote vinavyochelewesha maendeleo ya sekta ya viwanda na kuhimiza sekta binafsi kuchangamkia fursa za kuwekeza katika viwanda badala ya kubaki ikilalamikia changamoto inazokumbana nazo.

Send this to a friend