Rais Dkt Magufuli awakingia kifua Watendaji wa Kata
Rais Dkt Magufuli amewapongeza Watendaji wa Kata kwa kuiwakilisha vizuri Serikali katika Kata zao na amewahakikishia kuwa Serikali inatambua na inathamini uwepo wao na majukumu wanayoyatekeleza.
Rais ameyasema hayo leo tarehe 02 Septemba, 2019 alipokutana na Watendaji wa Kata zote hapa nchini katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katika Mkutano huo, Rais Magufuli amesikiliza maoni, kero na ushauri kutoka kwa Watendaji Kata wa Mikoa yote hapa nchini na kutoa majibu na maelekezo mbalimbali kwa watendaji na viongozi wa Serikali.
Katika mkutano huo, amewaagiza viongozi wa Wilaya, Mikoa na Wizara kuhakikisha Watendaji wa Kata hawanyanyaswi wakati wakitekeleza majukumu yao ya kusimamia ulinzi na usalama, maendeleo ya wananchi na kutekeleza maelekezo mbalimbali ya Serikali na kwamba hatosita kuchukua hatua dhidi ya viongozi na watendaji wakiwemo Maafisa Utumishi na Wakurugenzi wenye tabia ya kufanya unyanyasaji huo.
Hata hivyo, Mhe. Rais Magufuli amewataka Watendaji wa Kata kutowanyanyasa wananchi hasa wanyonge, kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na taratibu na kuhakikisha wanawatembelea wananchi ili kusikiliza na kutatua kero zao badala ya wananchi hao kusubiri mpaka watembelewe na viongozi wa Kitaifa.
Amewataka kufuatilia na kutoa taarifa juu ya miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika Kata zao katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, maji, barabara na miundombinu mingine pamoja na kusimamia vizuri ardhi.
“Usikubali mradi unatekelezwa kwenye kata yako wewe hujui, na usikubali mradi uhujumiwe kwenye kata yako na wewe upo, ukiona fedha zinachezewa toa taarifa, Mtendaji wa Kata ndio mwakilishi wa Rais kwenye Kata yako, wewe ndio bosi kwenye kata” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Rais Magufuli amewataka Watendaji wa Kata kuhakikisha wanawasimamia watumishi wote wa Serikali katika Kata zao, kujiepusha na vitendo vya rushwa na kushirikiana kwa karibu na Watendaji wa Vijiji katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Serikali.