Waziri wa Ulinzi wa Kenya, Aden Duale amesema kwamba Rais Mstaafu, Uhuru Kenyatta na jamaa zake wametuma wajumbe kwa serikali wakitaka waachwe peke yao.
Jina la Uhuru limekuwa kwenye vichwa vya habari wiki za hivi karibuni baada ya baadhi ya wanasiasa wa Kenya Kwanza kumshutumu kwa kuhamasisha maandamano ya kupinga serikali yanayoendelea yakiongozwa na kiongozi wa Azimio la Umoja, Raila Odinga.
“Ndio familia tajiri zaidi barani Afrika na wametuma wajumbe kwamba Rais wa zamani na familia yake waachwe peke yao,” amesema Duale.
Kenya: Waandamanaji wavamia shamba la Rais Kenyatta
Kulingana na Waziri wa Ulinzi, Serikali haiwezi kutoa hakikisho kwamba itamwacha Uhuru na familia yake peke yao kwani serikali ya sasa huenda ikalazimika kufanya ukaguzi katika serikali yake siku zijazo ili kubaini ikiwa ilitumia pesa za umma kwa kufuata matumizi na sheria husika.
Aidha, Duale amemshutumu Odinga kwa kuchochea maandamano dhidi ya serikali akidai kuwa anataka tu kuwa sehemu ya serikali ya Kenya Kwanza, lakini kupitia mlango wa nyuma.