Rais Kenyatta akosea hesabu mara mbili akihutubia Taifa

0
36

 

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amekosea hesabu mara mbili wakati akilihutubia Taifa jana, akitoa tathmini ya mafanikio aliyoyapata katika kipindi cha miaka nane ya uongozi wake, tangu mwaka 2013.

Kitendo hicho kimepelekea watumiaji wa mitandao ya kijamii kumkosoa.

Akitoa hotuba hiyo, alishukuru jeshi la nchi hiyo kwa kufufua Kiwanda cha Nyama Kenya (KMC) ambacho kilikuwa kikifanya vibaya kipindi cha nyuma.

Amesema chini ya jeshi, KMC ilikusanya shilingi za Kenya milioni 1 kila siku katika moja ya duka lake la mauzo na kwamba makusanyo hayo yalimaanisha shilingi milioni 30 kila mwezi, na shilingi bilioni 3.6 kwa mwaka katika duka moja.

Hesabu hiyo haiko sahihi kwa sababu kwa miezi 12, kiasi sahihi ni shilingi milioni 360 na sio bilioni 3.6 kama alivyosema.

Pia alikosea hesabu wakati akizungumzia kukua kwa ongezeko la uzalishaji umeme ambapo alisema alipochukua ofisi mwaka 2013, Kenya ilikuwa inazalisha megawati 1,300 na kwamba kiwango kimeongezeka mara mbili hadi megawati 2,600.

“Hii ina maana kuwa ni 325 megawati kila mwaka chini ya uongozi wangu,” alisema.

Kwa mara nyingine, hesabu hiyo si sahihi kwa sababu kama uzalishaji umeme umeongezeka kwa megawati 1,300 kwa kipindi cha miaka nane, hilo ni sawa na ongezeko la megawati 162 kwa mwaka, na sio megawati 325 alizotangaza.

Kenya inatarajia kufanya uachaguzi mkuu mwaka 2022 baada ya mihula miwili ya Rais Kenyatta kumalizika.

Send this to a friend