Rais Magufuli aeleza sababu ya kumteua tena Mwigulu Nchemba

0
60

Rais wa Tanzania Dkt Magufulia amesema kuwa amemteua tena Mwigulu Nchemba kwa sababu vijana wengi aliowateua hawajamuangusha hivyo anaamini na yeye atafanya kazi nzuri.

“Nimekuteua kwa mara ya pili kwa sababu naamini unaweza kutekeleza jukumu hili vizuri, na bahati nzuri vijana wengi niliowateua hawajaniangusha, kwa hiyo nakutakia heri katika kazi zako na Mungu akutangulie,” amesema Rais Magufuli.

Rais ametoa kauli hiyo mapema leo asubuhi wakati akimuapisha mbunge huyo wa Iramba Magharibi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Chato, mkoani Geita, Rais Magufuli amemuelekeza Mwigulu kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na mtangulizi wake, marehemu Balozi Dkt. Augustine Mahiga aliyefariki dunia Mei 01, 2020, na pia kushirikiana na viongozi wenzake katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya Serikali.

Rais Magufuli amerejea kauli yake ya kuwataka Watanzania kutokuwa na hofu kubwa dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19) na badala yake waendelee kuchukua tahadhari kama zinavyoelekezwa na wataalamu.

Send this to a friend