Rais Magufuli ampongeza kiongozi wa upinzani Malawi kwa kushinda Urais

0
42

Rais wa Tanzania, Dkt. Magufuli amempongeza kiongozi wa upinzani nchini Malawi, Dkt. Lazarus Chakware kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo.

Katika salamu zake za pongezi alizozitoa kwa niaba ya Watanzania wote, Rais Magufuli amemuahidi kiongozi huyo kuwa Tanzania itaendeleza uhusiano mwema na nchi hiyo.

“Kwa niaba ya Serikali na Watanzania wote naahidi kuendeleza uhusiano wetu wa kidugu, kirafiki na ujirani mwema hususani katika masuala ya uchumi na ustawi wa jamii,” ameandika Rais Magufuli kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Chakware amechaguliwa kuwa Rais katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Juni 23 mwaka huu kufuatia Mahakama ya Katiba kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa Mei, 21, 2019 ambayo yalimpa ushindi Rais Mstaafu, Peter Mutharika.

Februari mwaka huu mahakama hiyo ilitangaza uchaguzi uliofanyika 2019 ni batili kutokana na kukiukwa kwa sheria, na hivyo kuamuru kufanyika uchaguzi mpya.

Send this to a friend