Rais Magufuli amsamehe Mkurugenzi aliyenunua gari la gharama kubwa

0
14

Rais Dkt. Magufuli ametangaza kumsamehe Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kahama, Anderson Msumba aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma za kutumia fedha nyingi za halmashauri kununua gari la gharama kubwa, ameagiza gari hilo arejeshewe na amemuonya asirudie kufanya kosa kama hilo.

Aidha, amempongeza Msumba kwa ukusanyaji mzuri wa mapato na usimamizi wa fedha za mapato hayo zilizowezesha kujengwa kwa miradi mikubwa ikiwemo ofisi na hospitali kwa kutumia fedha za mapato ya ndani na kwa ubunifu wa kutoa viwanja bure kwa wawekezaji (kikiwemo kiwacha cha KOM Food Products) ambao baadaye watatoa tozo mbalimbali na kuongeza mapato ya halmashauri.

Rais Magufuli ametangaza uamuzi huo leo Januari 28, 2021 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Taifa wa Kahama.

Rais Magufuli amewataka Wakurugenzi na viongozi wa halmashauri, mikoa na wilaya nyingine hapa nchini kuwa wabunifu kama ilivyo katika Manispaa ya Kahama.

Wakati huo huo ameipandisha hadhi Halmashauri ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga na kuwa Halmashauri ya Manispaa baada ya kuridhishwa na kasi kubwa ya maendeleo ya mji huo na kuwepo kwa vigezo vya hadhi ya Manispaa.

Rais Magufuli kesho ataendelea na ziara yake ambapo atafungua mradi wa maji wa Kagongwa – Isaka.

Send this to a friend