Rais Magufuli amualika Waziri Mkuu wa Uingereza nchini, aomba aje na misaada

0
15

Rais wa Tanzania, Dkt. Magufuli amemualika Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson kuitembelea Tanzania kutokana na kuzidi kuimarika kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Dkt. Magufuli ametoa mualiko huo leo wakati wa uzinduzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Ihungo mkoani Kagera iliyokarabatiwa kwa ushirikiano kati ya Uingereza na Tanzania.

“Na utakapozungumza na uongozi wa Uingereza, napenda kumualika Waziri Mkuu wa Uingereza aje atembelee Tanzania, na akija huku aje na misaada mingine zaidi. Mgeni aje mwenyeji apone,” amesema Dkt. Magufuli akimwambia Balozi wa Uingereza nchini.

Aidha, ametumia nafasi hiyo kumpongeza Balozi wa Uingereza nchini Tanzania kwa namna ambavyo amekuwa akitekeleza majukumu yake na kumueleza kuwa tangu amekuja nchini, uhusiano wa nchi hizo umeimarika zaidi.

Amesema hajamsikia balozi huyo akiandika jumbe mitandaoni kuhusu Tanzania, badala yake amejikita kuchapa kazi, na hayo ndiyo yanayotakiwa.

“Kawafundishe mabalozi wenzako wajifunze namna ya kuishi vizuri na Tanzania ambayo haibabaishwi, inafanya kazi kutokana na misingi ya kimataifa,” amesema Rais.

Shule ya Ihungo imekarabatiwa kwa gharama ya TZS bilioni 10.9 ambapo Uingereza imetoa TZS bilioni 6.1.

Send this to a friend