Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amezungumza kwa njia ya simu na Rais Mteule wa Jamhuri ya Burundi Evariste Ndayishimiye na kumpongeza kwa uamuzi wa Mahakama ya Katiba nchini Burundi iliyoagiza Rais Mteule aapishwe haraka.
Katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli amemtakia heri Rais Mteule Ndayishimiye kuelekea kuapishwa kwake kuwa Rais wa Jamhuri ya Burundi kutakakofanyika hivi karibuni.
Rais Magufuli amemhakikishia Rais Mteule Ndayishimiye kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake wa karibu na Burundi kwa kuwa nchi hizo ni majirani, marafiki na ndugu wa kihistoria.
Rais Magufuli amerudia kumpa pole kwa msiba wa kuondokewa na Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza aliyefariki dunia tarehe 09 Juni, 2020 na amemueleza kuwa yeye na Watanzania wote wanaungana na Warundi katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.
Amemuomba kufikisha salamu zake za rambirambi kwa Warundi wote na kuwasihi waendelee kuwa watulivu na wastahimilivu.