Rais Magufuli ametoa wito kwa mahakama na Wizara ya Katiba na Sheria kufanya mabadiliko ya sheria na mifumo ya mahakama iliyorithiwa kutoka kwa wakoloni na ambayo imesababisha hukumu za mahakama kutolewa kwa lugha ya Kiingereza ambayo haifahamiki kwa Watanzania wengi, ili hukumu hizo zitolewe kwa lugha ya Kiswahili.
Rais ametoa wito huo mapema leo wakati akimuapisha Zepharine Nyalugenda Galeba kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, baada ya jana kutangaza kumpandisha cheo kutoka ngazi ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Magufuli amempongeza Jaji Galeba kwa kupandishwa cheo na amemtaka kwenda kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na taratibu za Mahakama, na kwa kumtanguliza Mungu.
Amesema hoja za kuwa Kiswahili hakina misamiati ya kutosha hazina mashiko kwa kuwa mwaka 1999 timu ya wanasheria iliandika kamusi ya sheria na pia lugha hiyo inatumiwa na watu wengi, mataifa na taasisi mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari vya kimataifa.
Galeba ameapishwa baada ya kupandishwa cheo na Rais Dkt. Magufuli ikiwa ni kutambua mchango wake wa kuthamini lugha ya Kiswahili ambapo alitumia lugha hiyo kutoa hukumu ya kesi ya mapitio namba 23/2020 kati mgodi wa dhahabu wa North Mara na mwananchi Gerald Nzumbi.