Rais Magufuli atangaza kufungua vyuo, na masomo kwa kidato cha sita

0
29

Rais wa Tanzania, Dkt Magufuli amesema kuwa kutokana na hali ya corona nchini kuendelea kuwa shwari, serikali imeamua kufungua vyuo vyote na kuanza masomo kwa wanafunzi wa kidato cha sita Juni Mosi mwaka huu.

Akitangaza azimio hilo Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma wakati akiwaapisha viongozi sita aliowateua hivi karibuni, Rais Magufuli amesema kuwa kwa wanafunzi wengine wa shule za sekondari, na wale wa shule za msingi wataendelea kubaki majumbani huku serikali ikiendelea kufuatilia hali itakavyokuwa.

“Kwa shule zingine za sekondari na msingi, tujipe muda kidogo tuangalie hii phase ya vyuo, kwa sababu wao ni watu wazima wanaojitambua tofauti na mtoto wa darasa la kwanza. Tutaona trend [hali] inavyokwenda,” amesema Rais.

Katika hatua nyingine ametangaza kuruhusu shughuli zote za michezo kuanzia Juni Mosi mwaka huu, huku akisema anaamini kwamba michezo [mazoezi] ni moja ya njia za kujikinga na corona.

“Michezo pia, nafahamu, kila mmoja anapenda michezo, sina uhakika kama kuna mwanamichezo kafariki kwa corona hapa Tanzania. Nimeamua nayo michezo kuanzia tarehe 1 mwezi 6 zianze maana najua kuna michezo mbalimbali ikiwemo ile ya majeshi na kuigiza,” amesema Rais.

Taasisi hizo za elimu zilifungwa katikati mwa mwezi Machi mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya hatua zilizochukuliwa na serikali kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Send this to a friend