Rais Magufuli atengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji

0
44


Rais wa Tanzania, Dkt. Magufuli amemteua Luteni Kanali Patrick Kenani Sawala kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.

Luteni Kanali Sawala anachukua nafasi ya Bw. Juma Njwayo ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Uteuzi wa Luteni Kanali Sawala unaanza leo tarehe 30 Julai, 2020.

Katika taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, haijaieleza sababu ya utenguzi huo, lakini inaweza kuhusishwa na malalamiko ya wananchi wa eneo hilo waliyoyatoa kwa Rais Magufuli leo.

Akiwa njiani kurejea Dar es Salaam, Rais Magufuli alisimama na kuzungumza na wananchi wilayani humo, ambapo miongoni mwa mambo waliyomueleza ni pamoja na ukosefu wa choo katika soko.

Katika hali ya kuonesha kukerwa na utendaji wa wasaidizi wake, Rais Magufuli aliwataka wananchi kutumia choo kilichopo kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Wilaya hadi hapo watakapotengeneza vyoo sokoni hapo.

Send this to a friend