Rais Magufuli atengua uteuzi wa RC Ole Sendeka, Prof. Mkumbo, ateua viongozi wapya

0
40

Rais wa Tanzania, Dkt. Magufuli amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali kama ifuatavyo;

Kwanza, amemteua Dkt. Jumanne Fhika kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe. Kabla ya uteuzi huo, Dkt. Fhika alikuwa Ofisi ya Rais na anachukua nafasi ya Bw. Christopher Ole Sendeka.

Pili, amemteua Dkt. Aloyce Nzuki kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Kabla ya uteuzi huo, Dkt. Nzuki alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na anachukua nafasi ya Prof. Adolf Mkenda.

Tatu, amemteua Mhandisi Anthony Sanga kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji. Kabla ya uteuzi huo, Mhandisi Sanga alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na anachukua nafasi ya Prof. Kitila Alexander Mkumbo.

Nne, amemteua Dkt. Allan Kijazi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Dkt. Allan Kijazi anachukua nafasi ya Dkt. Aloyce Nzuki aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, na pia Dkt. Allan Kijazi ataendelea kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Tano, amemteua Mhandisi Nadhifa Kemikimba kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji. Kabla ya uteuzi huo, Mhandisi Nadhifa Kemikimba alikuwa Mkurugenzi katika Wizara ya Maji na anachukua nafasi ya Mhandisi Anthony Sanga ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji.

Sita, amemteua Bw. Fadhili Mohamed Juma kuwa Mkuu wa Wilaya ya Geita Mkoani Geita. Kabla ya uteuzi huo, Bw. Juma alikuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Lindi na anachukua nafasi ya Josephat Paulo Maganga ambaye amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma. Bw. Josephat Paulo Maganga anachukua nafasi ya Bw. Patrobas Katambi.

Wateule wote wawepo Ikulu, Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 20 Julai, 2020 saa 4:00 asubuhi.

Send this to a friend