Rais Magufuli awalilia waliofariki mkoani Singida

0
40

Rais wa Tanzania, Dkt. Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia za watu 14 waliofariki dunia katika ajali ya barabarani iliyotokea Disemba 13, 2020 saa 9:30 alasiri katika Kijiji cha Mkiwa, Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Ajali hiyo imetokea katika barabara kuu ya Singida – Dodoma ambapo basi dogo lililokuwa limebeba watu waliokuwa wametoka Mwanza kwenda Itigi (Wilaya ya Manyoni) liligongana uso kwa uso na lori la mizigo lililokuwa linatoka Dar es Salaam kwenda Kahama (Mkoani Shinyanga) na kusababisha vifo hivyo na majeruhi 3.

Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi kufikisha salamu zake za pole kwa wafiwa wote, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo hivyo na amesema anaungana na familia hizo katika kipindi hiki cha majonzi.

“Nawapa pole wafiwa wote, Mwenyezi Mungu awatie nguvu, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na wapendwa wenu, nawaombea Marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, amevitaka vyombo vyote vinavyosimamia usalama wa barabarani, kuongeza jitihada za kuthibiti ajali hasa katika kipindi hiki cha kufunga mwaka ambapo kumekuwa kukitokea ajali nyingi za barabarani, na pia amewataka watumia barabara wote kuwa makini na kujiepusha kuvunja sheria na taratibu za barabarani.

Send this to a friend