Rais Magufuli awapa siri viongozi wa kimataifa namna ya kuishinda COVID-19

0
39

Rais wa Tanzania, Dkt. Magufuli ametoa wito kwa viongozi wa mataifa mbalimbali duniani kukubali kumweka Mungu mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Korona badala ya kutegemea nguvu za binadamu pekee.

Amesema upendo na miujiza ya Mungu kwa Tanzania inajidhihirisha katika kipindi hiki ambapo dunia inapita katika wakati mgumu wa janga la ugonjwa wa Korona (Covid-19) ambapo maelfu ya watu wanaendelea kupoteza maisha kila siku, lakini Tanzania imeepushwa na janga hilo na maisha ya Watanzania yanaendelea kama kawaida.

Dkt. Magufuli amesema hayo katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Imakulata, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma aliposhiriki Misa Takatifu ya Krismasi ambayo ni maadhimisho ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Amewaomba Watanzania wote waendelee kumshukuru na kumuomba Mungu aendelee kulilinda Taifa lao dhidi ya ugonjwa huo, na kuwaombea wananchi wa Mataifa mengine waepushwe na Korona.

Pamoja na kuwatakia heri ya Krismasi, Rais Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kuchapa kazi za uzalishaji mali ili kuendelea kujenga Taifa lao pamoja na kuhakikisha wanamtanguliza Mungu kwa kila jambo.

Send this to a friend