Rais Magufuli awataka Watanzania kujikinga na Corona

0
11

Rais Dkt. Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona kama zinavyoelekezwa na wataalamu wa afya na amefafanua kuwa Serikali haijazuia matumizi ya barakoa katika kujikinga kuambukizwa virusi vya Korona.

Amesema hayo alipoaungana na waumini wa Parokia ya Mtakatifu Petro, Oysterbay jijini Dar es Salaam kusali Misa Takatifu ya Jumapili (Dominika ya 1 ya Kwaresma) ambapo amewataka wananchi kutumia barakoa zinazotengezwa hapa nchini zikiwemo za Bodi ya Dawa (MSD) au zinazotengezwa na Watanzania wenyewe kwa kuwa barakoa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi zina mashaka ya kuwa sio salama.

Rais Magufuli amesisitiza kutumia njia za asili za kukabiliana na magonjwa ya kupumua ukiwemo ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kujifukiza (kupiga nyungu).

Aidha, amewataka Watanzania kuondoa hofu inayopandikizwa ambayo ina madhara zaidi, na amesisitiza kuendelea kumtumaini na kumtanguliza Mwenyezi Mungu kwa kuwa njia za kujikinga kwa barakoa, kutogusana na kutokaribiana (social distancing) pamoja na kujifungia majumbani (lockdown) vimeonekana kutokuwa suluhisho la uhakika kwani mataifa yanayofanya hivyo watu wake wanapoteza maisha kwa maelfu ikilinganishwa na hapa Tanzania.

Send this to a friend