Rais Magufuli azuia kubomolewa hoteli ya Sugu mkoani Mbeya

0
39

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema kuwa Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amesema hakuna mtu yeyote atakayebomoa hoteli ya aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini kupitia CHADEMA, Joseph Mbilinyi (Sugu) inayodaiwa kujengwa kwenye chanzo cha maji.

Chalamila amesema hayo wakati akiwa na mbunge huyo mstaafu pamoja na viongozi wa mkoa, ambapo ameeleza zaidi kuwa Rais amesema Sugu ni muwekezaji kama walivyo wawekezaji wengine.

“…. huyu ni mwekezaji kama wawekezaji wengine. Na ikiwezekana amedai kama tuna viwanja vingine upande huu wa uzunguni basi moja ya watu wanaotakiwa kufaidika navyo ni pamoja na Sugu ambaye amekwisha ananza kuwekeza hapa,” amesema Chalamila.

Aidha, amesema kuwa mchakato wa ujenzi wa hoteli hiyo ulifuata taratibu na kuwa ilianza kupimwa ardhi na ina hati, watu wa mipango miji na wanaohusika na upimaji walishapima maana yake hadi mkurugenzi wa halmashauri anafahamu eneo hilo, hivyo kama walitoa hati kwenye eneo lenye chanzo cha maji, tayari hoteli imejengwa.

“Hoteli hii watu wa NEMC wanaijua, watu wa Osha wanaijua, watu wa halmashauri wanaijua, mkuu wa mkoa anaijua, TRA wanaijua sasa kama wote tunaijua leo iweje tuseme iko kwenye maji, wakati inajengwa walikuwa wapi, wakati tunapima ardhi ilikuwa wapi au mto haukuwepo umekuja leo.”

Ameongeza kuwa, muwekezaji huyo ameyaacha maji yanaendelea kutiririka bila vikwazo na ametaka suala hilo lisipelekee mvurugano wa kisiasa kwani yeye anaamini Sugu ataendelea kutunza maji hayo.

Kwa upande wake Sugu amesema kuwa anaamini ujumbe uliobebwa kwenye salamu za Rais utasaidia kuleta kujiamini hata kwa wafanyabiashara wengine, kama itatokea nafasi ya kuwekeza zaidi Mbeya.

Ameongeza kuwa wakati wote hakuwa na wasiwasi kwa sababu ana nyaraka zote muhimu za ujenzi wa hoteli hiyo kwa sababu haikuota tu kama uyoga.

Send this to a friend