Rais Magufuli: Hospitali ya Rufaa ya Kanda, Chato ijengwe kwa pamoja, sio kwa awamu

0
21

Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufili ameiagiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuhakikisha Hospitali ya Rufaa ya Kanda, Chato inajengwa kwa pamoja na si kwa awamu kama ilivyo sasa.

Rais Magufuli ametoa maelekezo hayo leo mara baada ya mgeni wake, Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi kuweka jiwe la msingi katika hospitali hiyo inayotarajiwa kuhudumia takribani wananchi milioni 14.

Amesema kila mara akiwasiliana na Rais Nyusi hataweza kumwambia kuwa hospitali hiyo haijakamilika kwa sababu inajengwa kwa awamu, hivyo akataka awamu zote zijengwe kwa pamoja.

“… nitawabana kweli kweli wizara ya afya ili hospitali hii ikamilike mapema. Mambo ya kusema awamu ya kwanza, awamu ya pili, awamu ya tatu, hapana. Awamu zote zipigwe mara moja ziweze kumalizika,” ameagiza Rais Magufuli.

Awali akitoa taarifa kuhusu mradi huo, Waziri wa Afya, Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa awamu ya kwanza ambayo inagharimu TZS bilioni 16 ikihusisha ujenzi wa majengo ya huduma za wagonjwa imefikia asilimia 90.

Awamu hiyo ilianza Septemba 2017 na tayari serikali imetoa TZS bilioni 14 huku mkandarasi ikitarajiwa kikabidhi majengo hayo Machi 2021.

Aidha, Dkt. Gwajima amesema ujenzi wa awamu ya pili ambao utahusisha wodi za radiolojia, upasuaji wa mifupa na magonjwa ya ndani umefikia asilimia 37. Ameongeza kuwa, awamu hii unagharimu TZS bilioni 14 na tayari serikali imetoa TZS bilioni 4.1.

Awamu ya tatu ya ujenzi bado haijaanza na itahusisha ujenzi wa majengo ya upasuaji, utakasaji vifaa, huduma za kufua, huduma za kuhifadhi maiti na huduma za afya ya uzazi.

Mradi wote ukikamilika utakuwa na uwezo aa kuhudumia wagonjwa 700 hadi 1,000 kwa siku kutoka mikoa ya Geita, Rukwa, Kigoma, Tabora na sehemu za mikoa ya Shinyanga na Mwanza.

Kwa upandr wake Rais Nyusi ameipongeza serikali kwa ujenzi huo na kusema ni zawadi kwa Msumbiji kupewa nafasi ya kuweka jiwe la msingi. Pia amesema ziara yake ya siku mbili nchini inahusisha kufanya mazungumzo kuhusu maendeleo ya mataifa hayo mawili, usalama na masuala ya kiplomasia.