Rais Magufuli kuteua Naibu Waziri mpya wa Madini baada ya wa awali kushindwa kuapa

0
62

Rais wa Tanzani, Dkt. Magufuli amesema atateua Naibu Waziri mwingine wa madini baada ya Francis Ndulane, aliyekuwa ameteuliwa kushika wadhifa huo kushindwa kuapa kwa ufasaha mapema leo.

Rais Magufuli ametoa uamuzi huo wakati akizungumza mara baada ya kuwaapisha mawaziri 21 na naibu mawaziri 22 katika Ikulu Chamwino jijini Dodoma.

Ndulane ambaye kitaaluma ana Shahada ya Uzamili ya Uhasibu na Fedha kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe ameshindwa kuapa kwa ufasaha baada ya kujaribu mara tatu, na hivyo kutakiwa kurudi kwenye kiti kupisha wengine waendelee kuapa.

“Nafikiri hii nafasi tutateua mtu mwingine anayeweza kuapa vizuri, ambaye ataweza kusoma vizuri documents [nyaraka] za madini zikija ofisini. Na tutacheki vizuri digrii yako,” amesema Dkt. Magufuli

Pia amesema kuwa atachunguza digrii yake, hukua kitolea mfano kuwa kumewahi kuwepo mbunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyefukuzwa kwa kuwa na vyeti feki.

Aidha, Rais Magufuli amewapongeza wote walioapishwa kushika nyadhifa hizo na amewataka kwenda kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu na kutanguliza maslahi ya Taifa, kwa kuwa Watanzania wana matumaini makubwa na Serikali yao.