Rais Magufuli kuvunja Bunge la 11 kesho

0
28

Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema kuwa Rais wa Tanzania, Dkt. Magufuli anatarajia kulihutubia na kulivunja Bunge la 11 jijini Dodoma kesho Juni 16, 2020.

Bunge hilo lilifunguliwa na Rais Magufuli Novemba 20, 2015 baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Akifungua Bunge hilo, Rais Magufuli aliainisha viapaumbele kadhaa vya serikali yake ikiwemo kupambana na rushwa, kukusanya kodi, kupunguza urasimu katika kutoa huduma Serikalini, kuboresha huduma za afya, elimu, miundombinu ya barabara, madaraja na reli na kufufua Shirika la Ndege (ATCL).

Katika hotuba yake Rais atazungumzia mafanikio yaliyofikiwa na Serikali. Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kufufua ATCL kwa kununua ndege 11 ambapo ndege nane zimeshaanza kazi ndani na nje ya nchi, elimu imeboreshwa kwa kujenga na kukarabati shule na vyuo mbalimbali, kujenga zaidi ya vituo 360 vya afya, ujenzi wa hospitali 70 za wilaya, kuongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 hadi bilioni 270 na kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kodi toka shilingi bilioni 800 kwa mwezi hadi wastani wa shilingi trilioni 1.5 kwa mwezi na kuongezeka kwa upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijijini.

Send this to a friend