Rais wa Tanzania, Dkt. Magufuli amekwenda kutoa pole kwa familia ya Balozi Mstaafu Job Lusinde aliyefariki dunia Julai 7, 2020.
Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amekwenda nyumbani hapo akitokea Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete Jijini Dodoma ambako ameongoza Kikao cha Kamati ya Maadili na Usalama na Kikao cha Kamati Kuu ya CCM.
Akiwa nyumbani kwa Marehemu Balozi Lusinde, Rais Magufuli amekutana na Mjane wa Marehemu, Sara Lusinde, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu ambapo ameeleza kuguswa na kifo hicho na kwamba daima atamkumbuka kwa mchango wake alioutoa akiwa Waziri wa Ujenzi, ushauri wake mzuri na moyo wake wa upendo na ukweli.
Rais Magufuli ameeleza kuwa wakati wa utumishi wake Balozi Mstaafu Lusinde alikuwa mzalendo wa kweli, mchapakazi na aliyetetea maslahi ya Tanzania nchi ya nchi, na kwamba hata alipostaafu aliisemea vizuri Dodoma.
Amewataka wafiwa wote kuwa wastahimilivu na kumpuzisha salama hapo kesho tarehe 10 Julai, 2020 atakapozikwa.
Msiba wa Balozi Mstaafu Lusinde upo nyumbani kwake Kilimani Jijini Dodoma.