Rais Magufuli: Mzee Kikwete aliwatwanga marafiki zake akanipitisha mimi

0
37

Chama cha Mapinduzi (CCM) leo kimepitisha jina la Dkt. John Pombe Magufuli kuwa mgombea Urais wa Tanzania kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Zoezi la kupitisha jina hilo limemaliza katika ukumbi wa chama hicho mjini Dodoma ambapo limepitishwa kwa asilimia 100 baada ya wajumbe wote 1,822 waliohudhuria mkutano mkuu wa chama hicho kupiga kura za ndiyo.

Akizungumza baada ya zoezi hilo, mbali na mambo mengi aliyosema Rais Dkt Magufuli amesema kuwa kama isingekuwa Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete, yeye asingekuwa Rais kwa sababu Mzee Kikwete ndiye aliyempitisha baada ya kuwatwanga marafiki zake.

“Mimi nisingekuwa Rais bila Mzee Kikwete. Yeye ndiye aliyenipitisha mimi, akawatwanga hadi rafiki zake akanipitisha mimi. Kwenye uongozi hakuna urafiki, unatanguliza maslahi mapana ya taifa mbele,” amesema kiongozi huyo.

Rais Magufuli amebainisha kuwa hata wakati marais wastaafu wanapitishwa wapo watu waliotwangwa ili wao kupita na kwamba siku zote maslahi ya taifa yanatakiwa kuwa mbele.

Katika hatua nyingine Rais Dkt Magufuli amemteua kwa mara ya pili Makamu wa Rais, Samia Suluhu kuwa mgombea mwenza ambapo amesema mwanamama huyo ni mtii, mchapakazi na mzalendo wa kweli.

Send this to a friend