Rais Magufuli: Sitabadilisha wakuu wa mikoa na wilaya, wamechangia ushindi

0
12

Rais wa Tanzania, Dkt. Magufuli amesema kuwa hana mpango wa kubadilisha wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, makatibu wakuu, na kwamba hao waliopo sasa wataendelea kutumikia nafasi hizo.

Dkt. Magufuli amesema hayo leo Ikulu Chamwino jijini Dodoma wakati akimuapisha Dkt. Adelardus Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo amesema kuwa mabadiliko yatatokea endapo tu utendaji wa kiongozi husika utakuwa hauridhishi au astaafu ay aamue kujiuzulu.

Amesema amelazimika kulizungumza hilo ili kuwaondoa hofu watendaji hao ambao baadhi wameanza hadi kumtumia jumbe fupi (sms) wakimuambia “Mheshimiwa Rais nimejitahidi katika kipindi changu.”

Amewataka viongozi hao kuendelea kuchapa kazi na kwamba alianza nao na atamaliza nao, na yeye hakusema kwamba kipindi cha wateule hao kinaisha akiapishwa kwa muhula wa pili.

Aidha, amedokeza kuwa mabadiliko yatakuwepo kwa mawaziri na kuwa baadhi ya waliokuwepo hawatorudi badala yake atateua wengine kwani wigo wake wa kuteua umekuwa mpana zaidi.

“Mabadiliko yatakayokuwepo ni kwenye nafasi tu zile za uwaziri ambazo zenyewe tulienda kuomba upya. Wapo watakaorudi wapo ambao hawatorudi, tena siku hizi options (machaguo) ni kubwa, nina wabunge 264, kwa hiyo uchaguzi ni mkubwa zaidi,” amesema Dkt. Magufuli.

Mbali na utendaji mzuri wa watumishi hao ambao amesema ulichangia chama hicho kupata ushindi wa asilimia 84.4 kwenye uchaguzi mkuu uliopita, Dkt. Magufuli amesema shughuli ya kuapisha inachosha, na kwamba hawezi kuifanya kila akiingia madarakani.

Send this to a friend