Rais Magufulia amemsamehe aliyemfukuza kwa tuhuma za ubadhirifu

0
44

Rais wa Tanzania, Dkt Magufuli ametangaza kumsamehe aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye baada ya kiongozi huyo kumuomba msamaha mara kadhaa.

Rais ametangaza msamaha huo wakati akizindua jengo la jeshi hilo jijini Dodoma, ambapo mbali na Andengenye ametangaza pia kuwasamehe maafisa wengine wa jeshi hilo ambao wanatuhumiwa kuhusika kwenye ubadhirifu wa fedha.

Januari 23 mwaka huu Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Andengenye na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, kufuatia mkataba mbovu ambao jeshi hilo liliingia na Kampuni ya Romania kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali. Wakati huo huo aliridhia barua ya kujiuzulu ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Jacob Kingu.

Jeshi la Zimamoto lililiingia mkataba huo wenye thamani ya shilingi trilioni 1 bila kufuata sheria, kwani zabuni hiyo haikuwa imepangwa kwenye bajeti, wala haikupitishwa na bunge.

Akizungumza wakati akitangaza msamaha huo Rais alisema kwamba licha ya kwamba amemsamehe, lakini hatomrejesha kwenye jeshi hilo, badala yake atapangiwa kazi sehemu nyingine.

Hatma ya mkataba huo bado haijafahamika, lakini tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imewahoji viongozi kadhaa wa jeshi la zimamoto na wizara ya mambo ya ndani.

Send this to a friend