Rais Samia Suluhu Hassan amesema migogoro baina ya wakulima na wafugaji haina tija kwa taifa kwani inaweza kuleta machafuko na kulidhoofisha taifa.
Ameyasema hayo wakati akizindua Kampeni ya Tutunzane inayolenga kumaliza migogoro ya ardhi wilayani Mvomero ikihamasisha upandaji wa malisho ya mifugo, uchimbaji wa visima na malambo katika mashamba binafsi ya wafugaji pamoja na kuhamasisha wananchi kuwa rafiki wa mazingira.
Aidha, Rais Samia amewasisitiza wakulima na wafugaji kuwa kwa mujibu wa katiba ya nchi, kila mtu ana wajibu wa kutenda shughuli zake kwa namna ambayo haitaingilia haki na uhuru wa watu wengine pamoja na maslahi ya umma ikiwemo kuvamia hifadhi za Serikali.
“Haki yako haitakiwi kwenda kuzingia haki ya mwenzio, ukihisi wanyama wako wana haki ya kula sio kwenye shamba la mwenzio wapeleke kwenye malisho wakale kama ni mbali lima malisho yako wanyama wale pale, kwahiyo tuheshimiane na kazi ziende vizuri,” amesema.