
Rais Samia Suluhu Hassan amesema barabara, madaraja na miradi mingine ya ujenzi inayoendelea mkoani Tanga, ina lengo la kuufungua Mkoa huo kiuchumi, kiutalii, kibiashara na kuiunganisha na dunia.
Akizungumza Wilayani Pangani mkoani Tanga kwenye ziara yake inayoendelea, Rais Samia amesema miradi hiyo kwa kuunganisha na bandari ya Bagamoyo, itauunganisha na shoroba tofauti za kiuchumi, na matokeo yake ni kuleta hali bora kwa watu wa Tanga na Tanzania kwa ujumla.
“Tunataka uchumi wa Pangani ubadilike, lakini pia tuna dhamira ya kuiunganisha Tanga na mikoa kadhaa au shoroba kadhaa, kanda kadhaa za kiuchumi. Daraja lile [la Pangani] linaunganisha kutoka Bagamoyo hadi mpaka wetu na Kenya,” amesema.
Aidha, Rais Samia Suluhu ameiagiza Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania, kuhakikisha inamalizia ujenzi wa kipande cha barabara kinachounganisha Wilaya ya Tanga na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Pangani chenye urefu wa kilomita nane.
Katika hatua nyingine, Rais Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi la upanuzi wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa mjini Tanga, ambapo amezihimiza taasisi za dini nchini kutumika kuimarisha maadili na kupinga matumizi ya dawa za kulevya, akisema athari zake zinaweza kuharibu nguvu kazi ya vijana na kudhoofisha maendeleo ya Taifa.