Rais mpya wa Burundi, Evariste Ndayishimiye amevionya vyama vya upinzani nchini humo kwamba havitapata nafasi, huku hakihoji ni ipi mantiki ya mtu yeyote kuipinga serikali.
Ndayishimiye ametoa kauli hiyo wakati akilihutubia taifa mara baada ya kuapishwa kuiongoza nchi hiyo Juni 18 mwaka huu, ambapo amevitaka vyama hivyo kufanya kazi pamoja na serikali.
Aidha, ameahidi kuwa atahakikisha kunakuwa na uhuru wa kujieleza pamoja na kulinda haki za binadamu.
Kuapishwa huko kwa haraka kwa kiongozi huyo kumekuja kufuatia agizo la Mahakama ya Katiba ya Burundi kuagiza aapishwe baada ya mtangulizi wake Rais Pierre Nkurunziza kufariki dunia ghafla juma lililopita baada ya kupata shambulio la moyo (heart attack).
Kwa mujibu wa ratiba Ndayishimiye alitarajiwa kutwaa madaraka Agosti mwaka huu kufuatia kutangazwa mshindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Mei 20, 2020, ambapo aligombea kupitia chama tawala.
Katika hotuba yake amevisihi vyombo vya habari pamoja na watetezi wa haki za binadamu kushirikiana na serikali katika masuala ya kitaifa, vinginevyo watakuwa wanawatumikia watu wengine na si raia wa Burundi.
Pia, amewataka raia wa Burundi waliopo katika nchi nyingine kama wakimbizi kurejea nyumbani, lakini amewaonya kuto jaribu kuidhoofisha nchi.