Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi amesema Muungano wa Tanzania umeleta faida nyingi za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa wananchi wa pande zote mbili za muungano.
Amesema hayo leo katika mdahalo wa kutathmini Nafasi ya Mwanamke wa Tanzania katika Miaka 60 ya Muungano wa Tanzania ulioandaliwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa dhamira njema ya waasisi wa taifa ya kuunganisha nchi mbili imeendelezwa na viongozi wa pande zote mbili za Muungano kwa kuudumisha, kuimarisha na kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizojitokeza hadi sasa na hivyo kuufanya uwe imara zaidi.
Aidha, amesema wanawake walikuwa na mchango mkubwa kufanikisha kufanyika kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo pia amewahamasisha kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika chaguzi zijazo.