Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza kuwa sekta ya sukari ni kipaumbele katika kilimo kwa Tanzania, akisema kuwa viwanda vya sukari ni vitovu vya kilimo na uchumi.
Rais Mwinyi ameyasema hayo alipofungua mkutano wa wazalishaji sukari wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar Airport.
Rais Mwinyi ameeleza kuwa Tanzania imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari akisisitiza kuwa serikali inafanya juhudi kubwa kuhakikisha sekta hiyo inakua na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa taifa.
Aidha, ametoa rai kwa nchi za SADC kutumia fursa zilizopo kwa kuweka mazingira bora zaidi ya uwekezaji ili kukuza uzalishaji wa sukari.