Rais Mwinyi: Ziara ya Uingereza imekuwa na manufaa makubwa kwa Zanzibar

0
5

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi ameeleza kuwa ziara yake Uingereza imekuwa na manufaa makubwa kwa Zanzibar kwani wawekezaji wengi wameonesha dhamira ya kuwekeza nchini.

Dkt. Mwinyi amesema hayo alipozungumza na waandishi wa Habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume baada ya kuwasili nchini akitokea Uingereza alikohudhuria Mkutano wa Jumuiya ya Madola wa Masuala ya  Biashara na Uwekezaji uliojikita katika ajenda ya Uchumi wa Buluu.

Aidha, Dkt. Mwinyi amesema uchumi wa Zanzibar umeendelea kukua kila mwaka   ambapo sasa umefikia zaidi ya asilimia 7.

\Vilevile Dkt. Mwinyi amesema ukuaji huo wa uchumi utaendelea kukua zaidi kutokana na juhudi zinazochukuliwa na Serikali za kuwa na sera bora na kuzitangaza fursa pamoja na   kuwakaribisha wawekezaji zaidi wa mataifa mbalimbali kuwekeza nchini.

Akizungumzia suala la  Wazanzibar Wanaoishi nje ya Nchi (Diaspora), amesema mchakato wa kuwapatia hadhi maalum umefikia pazuri kwani tayari umewasilishwa  Bungeni ili kupata ridhaa ya Bunge hilo ili nao wapate fursa za msingi ikiwemo ununuzi wa ardhi, bima ya usafiri na kutambulika kwa familia zao.