
Rais Samia Suluhu Hassan amewaahidi watanzania kuwa ataendelea kuwajibika kwao kwa kuilea Tanzania na kuharakisha huduma zote muhimu za kijamii kama sehemu ya majukumu yake ya msingi kama kiongozi mkuu wa nchi.
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wananchi wa Korogwe mkoani Tanga ikiwa ni sehemu ya ziara yake iliyoanza hapo Februari 23, 2025, ambapo pamoja na hayo amekagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo.
“Ahadi yangu kwenu, kama mama, nitaendelea kuilea Tanzania kama mtoto wangu, nitaendelea kusukuma huduma za jamii zote zinazotakiwa kwa watu kama maji, elimu, afya, umeme, kilimo, nitajitahidi kufanya kazi yangu kama imavyotakiwa na hii ndiyo ahadi yangu kwenu,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amesema Serikali ina mpango wa kuwavutia zaidi wawekezaji wakubwa na wenye tija ya uhakika katika kilimo cha chai, ili kutoa fursa kwa wakulima kupata nafasi ya kuuza mazao yao.
Katika hatua nyingine, Rais Samia akizungumza wilayani Lushoto, amemwagiza Waziri wa Maliasili na Utalii kuangalia uwezekano wa kufanya mapitio ya kanuni za fidia kwa wakulima wanaoharibiwa mazao yao mashambani na wanyama wa hifadhi ili fidia hizo ziweze kulipa jasho la wakulima hao.
Rais Samia ameongeza kuwa tangu awasili mkoani Tanga, amejionea utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ndani ya Mkoa huo, na kwamba matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo kwa kiasi kikubwa zimetumika vizuri.