Rais Samia Suluhu Hassan leo amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo.
Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma ambapo Rais Mstaafu Obasanjo ametoa salamu zake za rambirambi kwa Rais Samia kufuatia vifo vya waliokuwa Marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni Hayati Benjamin William Mkapa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli waliofariki dunia Julai 23, 2020 na Machi 17, 2021 mtawalia.
Obasanjo amempongeza Rais Samia kwa kupokea kijiti cha kuwa Rais wa Tanzania na amemtakia heri katika majukumu yake.
Aidha, katika mazungumzo hayo viongozi hao wamezungumzia hali ya usalama barani Afrika na umuhimu wa wakuu wa nchi kujadiliana na kutafuta suluhisho la migogoro hiyo ambayo inasababisha vifo vya watu wasio na hatia hasa wanawake na watoto.
Pia viongozi hao wamezungumzia masuala ya maendeleo hasa katika uchumi na kusisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuongeza ushirikiano na kuondoa vikwazo vya biashara na uwekezaji.