Rais: Polisi kuweni mabalozi wa kusimamia maadili

Rais Samia Suluhu Hassan ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kuendelea kuwa mabalozi wa kusimamia maadili na kuwa sehemu ya kukomesha vitendo vya kuomba na kupokea rushwa.
Ameyasema hayo wakati akishiriki Sherehe ya Kufunga Kozi ya Maafisa na Wakaguzi wa Jeshi la Polisi katika viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Polisi mkoani Dar es Salaam.
“Muda baada ya muda tunarushiwa ‘viclip’ na mimi nikirushiwa namrushia IGP, watu wako hao barabara fulani angalia, na nashukuru nikimrushia hachelewishi anachukua hatua hapo hapo. Kwahiyo nendeni kakomesheni mambo ya rushwa. Hamjafunzwa ili mpewe silaha zaidi za kwenda kukomesha watu kwenye mambo hayo, mmefunzwa kwenda kutoa majawabu kwenye yale ambayo jeshi letu linalalamikiwa,” amesema.
Aidha, Rais Samia ameagiza Jeshi la Polisi kulitazama zaidi eneo la usalama barabarani na kutengeneza namna ya kuwafanya madereva kuwa madereva wazuri na wenye sifa ili kupunguza ajali za barabarani.
“Muweke conditions [vigezo] ngumu za kumfanya mtu kuwa dereva. Najua kwa sasa hivi anayefanya ajali ya kwanza, ya pili, ya tatu ni kufutiwa leseni, kupunguziwa pointi kwenye leseni, lakini kuwe na vikwazo zaidi vya kumfanya mtu kuwa dereva na dereva makini,” amesema.
Rais Samia ameongeza kuwa Serikali inatambua changamoto ambazo maafisa na askari wanakumbana nazo na kwamba imeanza kutoa fedha kushughulikia changamoto zilizopo.
Mbali na hayo, Rais Samia amelipongeza Jeshi la Polisi chini ya Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Camillus Wambura kwa mabadiliko makubwa ndani ya jeshi hilo ikiwemo kuimarika kwa utendaji kazi wa polisi na nidhamu ndani ya jeshi hilo.