Rais Ruto alituhumu shirika la Kimarekani juu ya vurugu za maandamano

0
18

Rais wa Kenya, William Ruto amelituhumu shirika binafsi la Kimarekani, Ford Foundation, kwa kufadhili ghasia wakati wa maandamano ya kupinga serikali nchini humo.

Akizungumza Nakuru nchini humo, Rais Ruto amedai kuwa shirika hilo liliajiri wahuni ili kusababisha vurugu wakati wa maandamano hayo ambayo yalisababisha uharibifu wa mali na biashara na wengine kadhaa kupoteza maisha.

“Nataka niulize watu wa Ford Foundation watuambie hiyo pesa wanatoa, wanatoa ifanye fujo ndio wapate faida gani?” ameuliza huku akieleza kuwa “tutawaita na tutawaambia kama hawana nia ya kudumisha demokrasia nchini Kenya, kama watafadhili ghasia na machafuko, tutawaita na tutawaambia wachukue hatua au waondoke.”

Amesema kwamba serikali yake haitamnyamazia mtu yeyote anayewafadhili vijana wa Kenya kusababisha fujo mitaani wakati wa maandamano ya amani.

“Hatuoni umuhimu wa machafuko na uharibifu wa mali. Wale wanaofadhili vurugu hizo, tunawajua na nataka kuwaita wale wanaohusika na machafuko nchini Kenya, wale wanaofadhili vurugu Kenya, aibu kwao,” amebainisha Ruto.

Aidha, dakika chache baada ya mkutano wake wa hadhara, Rais Ruto ametumia akaunti yake ya X (zamani Twitter) kusisitiza madai yake, akilitaka shirika hilo kueleza ukweli kuhusu jambo hilo na kujibu madai hayo.