
Rais wa Kenya, William Ruto, amewaonya wananchi dhidi ya jaribio lolote la kuvuruga amani na utulivu wa taifa hilo, kuelekea maandamano yaliyopangwa kufanyika Jumatano, Juni 25, 2025.
Akizungumza Ikulu jijini Nairobi leo, Rais Ruto amewataka Wakenya kuwaheshimu na kuwaunga mkono maafisa wa polisi, akiwaita kuwa ni watu muhimu kwenye taifa hilo.
“Hakuna aliye juu ya sheria; huwezi kuwatisha Polisi. Huwezi kutumia nguvu, matusi au vitisho dhidi ya Polisi, kwa sababu unalitishia taifa letu. Hao ndio walinzi wetu wa mstari wa mbele,” amesema Rais Ruto.
Wakati huo huo, vijana wa Kenya wametangaza kuwa maandamano hayo pia yatalenga kuwakumbuka wale waliopoteza maisha wakati wa maandamano makubwa ya kupinga Muswada wa Fedha mwaka 2024.
Kwa mujibu wa makundi ya kutetea haki za binadamu, watu wasiopungua 60 waliuawa wakati wa maandamano hayo, huku wengi wakitekwa nyara na baadhi yao wakiendelea kupotea hadi sasa.








