
Rais wa Kenya, William Ruto, ameendelea kusimama imara katika ajenda yake ya kuimarisha uchumi na kupunguza gharama ya maisha, huku akiwapuuza vikali wakosoaji wanaodai kuwa nchi hiyo inashindwa kusonga mbele.
Rais Ruto amesema licha ya lawama na shutuma kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wa upinzani na wapinzani, serikali yake ina mpango mahsusi wa kuunda ajira, kupambana na mfumuko wa bei na kuhakikisha usalama wa chakula nchini.
“Tuna mpango wa jinsi ya kuunda ajira rafiki zangu. Hivyo basi, asiwadanganye mtu yeyote. Unajua unapowasikia baadhi ya watu wakizungumza ni kana kwamba Kenya ndiyo nchi mbaya zaidi duniani,” amesema Rais.
Ruto amesisitiza kuwa hatua na maamuzi aliyochukua ni magumu lakini ni muhimu kwa maendeleo ya taifa hilo. “Unaweza kusema unachotaka, lakini ukweli upo pale pale. Nimefanya maamuzi magumu kufika hapa, na sina majuto yoyote,” amesema.







