Rais Samia aagiza kuongezwa jitihada za kuokoa waliofunikwa mgodini Shinyanga

0
123

Rais Samia Suluhu Hassan ameielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na vyombo vya Usalama kupeleka misaada ya haraka na kuongeza jitihada za uokoaji kufuatia maafa yaliyotokea katika mgodi wa Nyandolwa, Kata ya Mwenge Wilaya ya Shinyanga Vijijini.

Ajali hiyo imetokea Agosti 11, 2025 baada ya ardhi kutitia wakati wafanyakazi na mafundi wakifanya ukarabati wa mashimo matatu katika eneo hilo ambapo takriban watu 25 walifunikwa ardhini huku wanne kati yao wakiokolewa.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mohamed Mhita, shimo la kwanza lilikuwa na mafundi 11, la pili lilikuwa na mafundi 8, na shimo la tatu lilikuwa na mafundi 6 ambao wanne kati ya mafundi 6 waliweza kuokolewa na mmoja kufariki baadaye.

Aidha, Mhita ameeleza kuwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na wachimbaji katika eneo hilo walifika na kuanza zoezi la uokoaji.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Rais Samia Suluhu amemtumia salamu za pole Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, kufuatia majanga hayo na kuwapa pole ndugu, jamaa na Watanzania wote kufuatia maafa hayo.

Send this to a friend