Rais Samia aagiza mifumo ya TEHAMA serikalini isomane

0
56

Rais Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inayosimamia sera ya TEHAMA kwa kushirikiana na wizara nyingine na taasisi husika kuhakikisha mifumo yote ya TEHAMA inayotumika ndani ya Serikali inasomana.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mkongo wa Mawasiliano wa Baharini wa 2Afrika pamoja na teknolojia ya kasi ya 5G ya mtandao wa Airtel mkoani Dar es Salaam amewaagiza watoa huduma yakiwemo mabenki, Wizara ya Elimu, Wizara ya Afya na wizara zote zinazotoa huduma kutumia namba moja itakayojumuisha taarifa zote za Mtanzania ili kurahisisha huduma.

“Tunataka kujuana nani ni nani, mwenyeji wa Tanzania ajulikane ni mwenyeji wa Tanzania, mgeni aliepo tujue huyu ni mgeni aliyepo. Mkitumia namba moja inayonitambulisha kila taasisi ikifungua ni namba ile ile ni Samia yule yule, na hii itatupunguzia ninapokwenda kutaka huduma kuambiwa leta hiki leta hiki, amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amesema Serikali ya Awamu ya Sita imejizatiti kuweka mazingira wezeshi kwa kutoa huduma za wawekezaji na kujenga miundombinu ya mawasiliano, pia inaendelea na jitihada za kukuza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa lengo la kujenga uchumi jumuishi wa kidigitali pamoja na kuboresha maisha ya wananchi mijini na vijijini.

Mbali na hivyo, Rais Samia amesema Serikali imepunguza gharama za kuweka mkongo kwenye hifadhi za barabara kutoka dola za marekani 1,000 [milioni 2.4] zilizokuwa zikilipwa awali hadi dola 100 [laki 2] ili mkongo huo uweze kusambazwa kwa haraka.

Machinga, bodaboda wamwagia sifa uongozi wa Rais Samia

Naye Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema kupitia mkongo huo kasi ya intaneti nchini itaongezeka kwa zaidi ya mara 10 ya sasa, utasaisdia katika jitihada za kushusha gharama za mawasiliano nchini na kukaribisha fursa ya wawekezaji kutoka kwenye makampuni makubwa pamoja na kutoa ajira kwa Watanzania.

“Kwa sasa mikongo yote tuliyonayo nchini ina wastani wa kasi ya 16 terabyte kwa sekunde, mkongo wa 2Afrika una kasi ya 180 terabyte kwa sekunde, mara 11.25 zaidi ya kile tulichonacho, hili jambo ni kubwa kwa mstakabali wa nchi yetu, amesema.

Pia ameahidi kutekeleza agizo la Rais la kufunga huduma ya inatenti ya bure katika vyuo na maeneo ya biashara, hasa walipo wafanyabiashara wadogo pamoja na usafiri wa mabasi ya mwendokasi ili kuendelea kukuza biashara na kurahisisha utoaji huduma.

Send this to a friend