Rais Samia aagiza ulinzi wa haki ya faragha ya kila mtu

0
39

Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza ulindwaji wa haki ya faragha ya kila mtu ambayo ni haki ya msingi ya binadamu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na sheria za kikanda na kimataifa.

Ameyasema hayo katika uzinduzi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi pamoja na mifumo ya usajili na malalamiko ya ukiukwaji wa misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi, hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

“Ibara ya 12 ya Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948 linayataka mataifa kuweka utaratibu unaohakikisha mtu yeyote haingiliwi katika faragha yake, familia yake, nyumbani au kwenye makazi yake wala kuvunjiwa heshima, utu na hadhi yake,” ameeleza.

Amesema mwaka 2015 Tanzania ilitunga sheria mbili zilizopendekezwa na jumuiya za kikanda ambazo ni Sheria ya Makosa ya Mtandao na Sheria ya Miamala ya Fedha, hivyo ilisalia kutunga Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ambayo tayari imefanyia kazi na kuzindua tume.

Aidha, katika hotuba yake, Rais Samia ametoa agizo na kuzisisitiza mamlaka husika kuhakikisha ifikapo Desemba mwaka huu mifumo yote ya Serikali iwe inasomana ili kurahisisha mawasiliano ndani ya Serikali.

Akizungumza kuhusu tume iliyozinduliwa leo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema “kuwepo kwa taasisi imara kama TCRA na sasa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ni moja ya vijenzi vinavyoifanya Tanzania kuwa nchi ya pili kwa usalama mtandaoni Barani Afrika.”

“Tukio hili la leo linaiingiza Tanzania katika orodha ya nchi za wastaarabu duniani wanaoheshimu utawala wa kisheria, wanaoheshimu ubinadamu, wanaoheshimu haki na wanaoheshimu faragha za watu na kuchangia katika jitihada za dunia kufanya ulimwengu wa mtandao kuwa salama,” amesema Nape.

Send this to a friend