Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan ameliagiza jeshi la polisi kuangalia upya utaratibu wa utoaji wa fomu ya matibabu ya polisi (PF.3) kwa watu wanaopata ajali, kwani utaratibu ulivyo sasa unasababisha watu wanafariki bila huduma.
Rais Samia amesema kuwa watu wengi wanafariki kwa sababu wanashindwa kupatiwa huduma kwa kukosa fomu hiyo ambayo ni sharti la kwanza kabla mtu aliyepata ajali hajaanza kuhudumiwa hospitalini.
Ameagiza utaratibu huo kubadilishwa na kwamba mtu apatiwe kwanza huduma za kitabibu ndio masuala mengine ya kipolisi yafuate, kwani mtu akiokotwa njiani amepata ajali, wazo la wasamaria hao sio kwenda polisi, bali hospitali.
Katika hatua nyingine amelitaka jeshi hilo kujikita katika kutoa elimu ya usalama barabarani badala ya kutumia sheria kukusanya fedha.
Amesema hilo baada Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro kusema kuwa kati ya Julai 2020 hadi Aprili 2021 wamekusanya TZS bilioni 50.1 zilizotokana na makosa mbalimbali.
Ili kudhibiti madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani, Rais ameliagiza jeshi hilo kuwa na mfumo ambao utasomeka nchi nzima ambao, mosi, utasaidia kujua dereva ametenda kosa gani, akiwa mkoa gani, tofauti na sasa ambapo dereva aliyetenda kosa Pwani, anaweza asitambulike mkoani Tanga.
Pili, mfumo huo utakuwa na utaratibu kwamba dereva akifikisha idadi fulani ya makosa atanyang’anywa leseni yake.
Ametumia jukwaa hilo kulipongeza jeshi la polisi kwa ukarabati na upanuzi wa kiwanda cha ushonaji kilichopo Bohari Kuu ya Jeshi Polisi, Kurasini Dar es Salaam ambacho amekizindua leo, na kuagiza majeshi mengine kutumia kiwanda hicho kushona sare zao, badala ya wao kufungua viwanda vyao.