Rais Samia aahidi kukuza zaidi ushiriki wa vijana kwenye kilimo

0
32

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kwa sasa sekta ya kilimo ndio chanzo kikuu cha ajira kwa vijana hivyo Serikali imeandaa mazingira bora kwa ajili ya kuwawezesha vijana katika kilimo ili kukuza uchumi wa nchi.

Akizungumza leo katika Mkutano Mkuu wa 53 wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-PF) uliofanyika Jijini Arusha, amesema Serikali inashiriki kwa kiasi kikubwa kuwekeza na kukuza biashara ya kilimo kwa vijana kupitia mpango ‘Building A Better Tomorrow’ ili kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana.

“Hivi sasa kilimo ndio chanzo kikuu cha ajira na mapato kwa takribani asilimia 61 ya idadi ya wakazi wa jumuiya ya SADC. Kwa hivyo hii ndiyo sekta ambayo serikali yetu inapaswa kuzingatia ipasavyo ili kutimiza dira ya SADC ya 2050, ajenda ya AU [Umoja wa Afrika]2063, na Ajenda ya UN [Umoja wa Mataifa] 2030,” amesema.

Rais Samia apongezwa kwa kukuza biashara na uwekezaji

Aidha, amesema licha ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kujiwekea mikakati na sera za kuboresha sekta ya kilimo, bado zinatajwa kuwa na njaa, hivyo ameeleza kuwa ni wakati wa nchi hizo zitumie mikakati na sera hizo ili kuufanya ukanda wa SADC kuwa mzalishaji na msambazaji mkubwa wa chakula Afrika na kwingineko.

Naye, Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amesema “Kama Bunge la SADC, tutafanya kazi kuhakikisha nchi zetu zinakamilishana badala ya kushindana katika sekta ya kilimo. Tunahitaji kuzalisha kile ambacho ni kizuri na kinachohitajika na majirani zetu, na pia kujifunza kutokana na uzoefu wa kila mmoja wetu.”

Send this to a friend