Rais Samia aahidi kushirikiana na taasisi za kidini kwenye sekta ya kilimo

0
36

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaangalia namna ya kushirikiana na kufanya kazi na taasisi za kidini kwenye sekta ya kilimo ili vijana wengi zaidi waingie kwenye sekta hiyo.

Ameyasema hayo wakati wa hafla ya ufunguzi wa jengo la Kitega Uchumi la Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika mkoani Dodoma ambapo amewaomba viongozi wa dini kuwahimiza waumini kufanya kazi kwa bidii na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotokana na kuhamishia Makao Makuu ya Serikali mkoani humo.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kuthamini mchago mkubwa unaotolewa na taasisi pamoja na mashirika ya kidini nchini. Mbali na kutoa huduma za kiroho ambazo zinachangia sana kujenga taifa la watu wenye uadilifu na uchaji Mungu, taasisi hizi zinasaidia sana Serikali katika kutoa huduma kwa wananchi hususani afya, elimu, maji na hata kilimo,” amesema.

Aidha, Rais Samia amewahimiza viongozi wa dini kuwafundisha vijana maadili mema na kuwakemea wale wote wanaotumia makanisa kufanya maovu pamoja na kuiweka Tanzania kwenye mikono ya Mungu.

“Nawasihi viongozi wa kanisa hili [Anglikana] na viongozi wote wa dini nchini kuendelea kuliweka taifa letu katika mikono salama ya Mwenyezi Mungu ili lidumu katika amani, umoja na mshikamano. Kamwe tusikubali kuyumbishwa na mtu yeyote yule asiyelitakia taifa letu mema,” Ameeleza.

Send this to a friend