Rais Samia aahidi Tanzania kuwa na umeme wa uhakika

0
7

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya awamu ya sita imetimiza kutoa huduma ya maji vijijini kwa asilimia 83 ikiwa ni pungufu ya asilimia mbili ambayo kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ni asilimia 85.

Kwa upande wa Miji Serikali imesema imefika asilimia 90 zikisalia asilimia 5 kama ambavyo Ilani ya CCM imeagiza.

Akizungumza wakati akihutubia viongozi pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma, amesema mpaka sasa, tayari vijiji vyote nchini vimefikiwa na umeme na kinachofanyika ni usambazaji wa umeme kwenye vitongoji, hivyo ana imani kuwa baada ya miaka mitatu, Tanzania yote itakuwa na umeme.

“Tunajenga njia mpya za kusafirisha umeme, tunajenga Station za kupooza umeme ili kufanya umeme utulie, kwa sababu umeme upo kwa wingi Bwawa limekamilika linazalisha karibu Megawati 2000, elfu moja naa zilikuwepo kabla, kwahiyo Tanzania kwa sasa tuna elfu tatu kama na mia sita, Umeme upo kwa wingi lakini mgao kuupeleka umeme ndio tatizo hiyo kazi tunaifanya kwa nguvu zote ili Tanzania yote wapate umeme wa uhakika,” amesema.

Aidha, amesema Serikali imepunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa madawa, ambapo zamani wagonjwa walilazimika kusafiri kutoka mikoani kwa ajili ya kufuata huduma Dar es Salaam, lakini hivi sasa huduma hizo zinapatikana katika Hospitali za mikoani.

“Tumepunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa madawa, supply [usambazaji] ya madawa sasa inakwenda vizuri na kwamba referrals [rufaa] zile za maradhi kuja Dar es Salaam na Benjamin Mkapa zinaishia Hospitali za mikoa, kwa sababu vifaa vyote, utaalamu wote, watumishi kila kitu kiko kule,” ameongeza.