Rais Samia aalikwa Vatican na Papa Francis

0
16

Rais Samia Suluhu anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa Vatican nchini Italia kuanzia Februari 11 hadi 12 mwaka huu kufuatia mwaliko wa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema lengo la ziara hiyo ni kukuza ushirikiano kati ya Tanzania na Vatican.

Tanzania na Vatican tangu mwaka 1960 zimekuwa zikishirikiana katika masuala ya elimu, afya, amani na kiroho.

“Kanisa Katoliki linakadiriwa kumiliki zaidi ya shule za chekechea 240, shule za msingi 147, shule za sekondari 245, vyuo vya ufundi 110, na vyuo vikuu 5 nchini Tanzania,” imeeleza taarifa iliyotolewa na wizara huku takribani taasisi za afya 473 zikiendeshwa na Kanisa Katoliki.

Tofauti za udini hazijawafanya viongozi hawa kushindwa kukaa pamoja na kujadili maslahi ya wananchi na uendelezaji wa ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.