Rais Samia aelekeza mashirika ya umma kufanya mabadiliko ya kiutendaji

0
71

Rais Samia Suluhu amewataka Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kutoa maoni yao ya namna wanavyotamani taasisi wanazoziongoza ziwe miaka 25 ijayo, na kusisitiza mashirika na taasisi hizo kuendelea kufanya mabadiliko ya kiutendaji ili kufikia malengo yaliyowekwa.

Ameyasema hayo wakati wa Ufunguzi wa Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kilichofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).

“Tunaposisitiza mabadiliko, ufanisi, mashirika yalete faida ni kulinda rasilimali za wananchi ambazo zimewekezwa ndani ya mashirika hayo, lakini pia ni kutengeneza lengo la kuundwa kwa mashirika haya. Kwa hiyo mabadiliko haya tunayafanya kwa nia njema kabisa ya kujenga nchi yetu,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amesisitiza mashirika ya umma kukumbuka kuwa uwekezaji nje ya nchi utakuwa na maana zaidi iwapo mashirika hayo yatajiimarisha ndani ya nchi kabla ya kuvuka mipaka ya nchi, na kuongeza kuwa mashirika hayo yajadili namna yatakavyoweza kuchangia sekta binafsi kuyafikia masoko ya kimataifa.

Mbali na hayo, Rais Samia amewapongeza wenyeviti na watendaji wa taasisi walioelewa madhumuni na dhamira ya serikali katika mageuzi ya utendaji na uendeshaji wa mashirika ya umma nchini.