Rais Samia aeleza alivyowahi kukamatwa na polisi usiku

1
55

Akifunga Mafunzo ya Uofisa Kozi Na. 01/2020/2021 (Warakibu Wasaidizi wa Polisi – ASP), Rais Samia Suluhu Hassan ametumia nafasi hiyo kutaka jeshi hilo lijirekebishe na kufanya shunguli zake kwa kufuata misingi na sheria za nchi.

Amiri Jeshi Mkuu amesema kuwa kumekuwepo na vitendo vya kutumia nguvu kupitiliza wakati wa ukamataji wa watu, na mara nyingine watu hukamatwa pasipokuwa na makosa ya msingi.

Ametolea mfano wa yaliyowahi kumkuta huko nyuma akiwa anafanya kazi serikalini kwamba alikamatwa na polisi saa saba usiku kwa sababu taa moja ya gari haikuwa inawaka bila ya yeye kujua, lakini alipoeleza hivyo, na kwamba asubuhi atatengeneza askari huyo hakukubali na kumlazimisha kumpeleka kituoni umbali wa 15km.

Mbali na hilo, amesema baadhi ya askari wamekuwa na  lugha zisizofaa na kueleza kuwa kuna wakati aliwahi kukamatwa kwa kutaka kugonga gari la polisi, alipofikishwa kituoni na kuandika maelezo, alisubirishwa kwa muda mrefu hadi giza likaingia, mbu wakaanza kumuuma. Askari akamwambia asiwaue mbu hao awaache wamnyonye damu kwani hawana shamba.

Pia amekemea vitendo vya rushwa na kueleza kwamba vinalichafua jeshi hilo ambalo lina kazi kubwa ya kuwalinda raia na mali zao.

Amehoji kuwa endapo yeye alikuwa serikalini anafanya hivyo, inakuwaje kwa mwananchi wa kaawaida?

Katika hafla hiyo maofisa 747 wamehitimu mafunzo hayo kwenye Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini, Jijini Dar es Salaam  kufikia ngazi ya Warakibu Wasaidizi wa Polisi ambapo awali walikuwa Wakaguzi wa Polisi. Mafunzo hayo yalianza Juni 18 mwaka huu ikiwa ni sehemu ya uamuzi wa Rais kuwapandisha vyeo watumishi wa polisi.

Send this to a friend