Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imeongeza uwazi katika mapambano dhidi ya rushwa pamoja na kuwekeza zaidi katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa huduma ambazo si lazima yawepo mawasiliano ya mtu kwa mtu ili kupunguza tatizo la kuzungumza na kupatana.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Rushwa barani Afrika, amesema tayari Tanzania inatumia TEHAMA katika michakato mbalimbali ikiwemo ya zabuni, usajili wa biashara, namba ya mlipa kodi na maombi ya kuunganishiwa umeme na mambo mengi mengine.
“Hata hivyo pamoja na jitihada hizo tunatambua kuwa bado jitihada zinahitajika kukabiliana na janga hili la rushwa kwa njia za kiuadilifu na ufanisi zaidi, hivyo tumeanzisha Divisheni ya Mahakama Kuu inayosikiliza kesi zinazowahusu washitakiwa wa makosa ya rushwa kubwa. Kuanzia mwaka wa Fedha 2019/20 hadi 2021/22, tulifanikiwa kuokoa na kudhibiti matumizi ya fedha yasiyostahili ya zaidi ya TZS bilioni 139 ambacho ni kiasi kikubwa kidogo kwa fedha za umma,” amesema
Aidha, amesema Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa ni mfumo wa kisheria unaoziwezesha nchi kushirikiana katika kuzuia vitendo vya rushwa, katika kuwachunguza watuhumiwa wa makosa ya rushwa pamoja na urejeshwaji wa mali zilizotokana na vitendo vya rushwa katika nchi husika, kubadilishana watuhumiwa wa makosa ya rushwa waliotoroka nchi zao na kubadilishana taarifa na ushahidi.
Rais Samiaa amesema mkataba huo umeweka misingi ya kisheria ya nchi za Afrika kushirikiana katika mafunzo ya kiweledi yanayohusu namna ya kuzuia na kupambana na rushwa na kupeana misaada ya kisheria pamoja na ushirikiano wa kiufundi katika kushughulikia kwa haraka maombi ya vyombo vilivyopewa jukumu la lazima la kuzuia, kutambua, kuchunguza na kuadhibu washtakiwa wa makosa ya rushwa.
Mbali na hayo, ameipongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mamlaka ya kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) kwa juhudi kubwa dhidi ya kupambana na rushwa pamoja na sekta binafsi, asasi za kiraia, vikundi vya kidini na wadau wengine wanaoshirikishwa katika mapambano hayo.