Rais Samia aeleza sababu za kuwavua uwaziri Lukuvi na Kabudi

0
46

Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza sababu ya kuwaondoa katika baraza la mawaziri viongozi wawili waandamizi, William Lukuvi na Prof. Palamagamba Kabudi waliokuwa mawaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Katiba na Sheria, mtawalia.

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowatea karibuni wakiwemo mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na manaibu wao, Rais Samia amesema anawahitaji karibu yake ili waweze kumsaidia majukumu mengine.

Akianza na Kabudi, amesema alifanya kazi nzuri kuongoza majadiliano kati ya mashirika na serikali, na hivyo jukumu kubwa analopewa sasa ni kuongoza timu ya majadiliano ambayo itahusika na mitakataba yote ya ubia kati ya mashirika na serikali.

“Kabudi amefanya kazi nzuri sana kusimamia majadiliano ya serikali na mashirika, na ndiyo kazi ninayotaka nimkabidhi sasa kindakindaki…Mashirika yote, kazi zote zitakazoingia ubia na serikali, Kabudi ataongoza hiyo timu. Kwa hiyo yeye ni baba mikataba, amesema Rais.

Kuhusu Lukuvi Rais amesema kwamba atakuwa Ikulu, lakini hakutaja kazi ambayo atakuwa akiifanya kwa maelezo kwamba ataitaja hapoa baadaye.

“Kaka yangu Lukuvi, yeye ana kazi na mimi, mtaisikia baadaye. Lakini namvuta Ikulu, kazi yetu ni kuwasimamia nyinyi.”

Amekanusha madai kwamba Lukuvi atagombea nafasi ya Spika wa Bunge na kusema kwamba, “Wengine wameanza kumletea [William Lukuvi] meseji za ajabu ajabu wakijua atagombea Uspika, hatogombea. Ana kazi na mimi.”

Viongozi hawa wawili ni baadhi tu ya waliiondolewa katika baraza la mawaziri kufuatilia mabadiliko yaliyofanyika Januari 8 mwaka huu. Wengine ni Prof. Kitila Mkumbo, Goeffrey Mwambe, Mwita Waitara.

Hafla ya uapisho imefanyika katika viwanja vya Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Send this to a friend