Rais Samia aeleza sababu za ukosefu wa maji Dar

0
48

Rais Samia Suluhu Hassan amesema sababu za kupungua kwa maji katika Mto Ruvu umechangiwa na uharibifu unaofanywa na baadhi ya wananchi ikwemo ukataji wa misitu unaosababisha vyanzo vya maji kukauka.

Ameyasema hayo leo katika Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia ilioyofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

“Kwanza tumeambiwa kwamba mkoa ule [Pwani] ndio unakata misitu kwa kiasi kikubwa, kwa hiyo vyanzo vya maji vinakauka. Vyanzo vidogo vidogo vilivyokuwa vikichangia maji ndani ya mto Ruvu vinakauka maji hayaendi, na yale yanayokwenda njiani huko unakuta watu wanaolima wameweka vizuizi maji hayawezi kutiririka,” amesema.

Kutokana na hayo Rais Samia ameiagiza Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar Es Salaam  (DAWASA)  kuondoa vizuizi vyote vilivyopo katika Mto Ruvu ili kuwezesha upatikanaji wa maji safi na salama kwa urahisi.

Aidha, amesema lazima nishati safi izingatiwe kwa maendeleo ya nchi, jamii na pia kulinda haki ya wanawake ambao ndio waathirika wakubwa zaidi wa nishati isiyo salama ya kupikia na kuwapunguzia athari zinazotokea.

Katika kongamano hilo amependekeza kuanzishwe kwa kikosi kazi cha kitaifa ambacho kitaratibu na kushughulikia nishati ya kupikia ili kuepusha athari hizo.

Send this to a friend